Historia

Historia Ya Wadigo

Una sababu zote za wewe mwenye kusoma kuifahamu Historia Ya Wadigo. Digo ni kabila linalopatikana katika mikoa wa Tanga na Pwani nchini Tanzania.
Wao ni sehemu ya jamii ya wabantu na lugha yao inaitwa Kidigo. Lugha hiyo, Kidigo, ina uhusiano wa karibu na lugha za Kisambaa na Kizigua. Kwa mujibu wa historia kwa njia ya simulizi na machapisho mbalimbali, awali Wadigo walikuwa wakiishi maeneo ya Digi na Kirau nchini Kenya. Hata hivyo, inadaiwa kuwa kabla ya hapo Wadigo walikuwa wakiishi eneo la Chungwaya lililopo katika nchi ya Mali, Afrika Magharibi.
Hivi sasa eneo hilo linaitwa Timbuktu. Hata hivyo, Martin Kayamba katika utafiti wake kuhusu Wadigo ambao ulichapishwa mwaka 1947 anasema kabila hilo linatokana na kabila maarufu la Wambokomu ambalo liliingia Kenya likitokea Afrika Magharibi kisha likasambaa katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa utafiti huo asili ya Wadigo wa sasa ni vita kati ya Wagala na Wasegeju iliyorindima karne ya 19. Wasegeju walipoona wanazidiwa nguvu katika vita waliomba msaada kutoka kwa Wambokomu ambao walikubali kusaidia rafiki zao.
 Pamoja na msaada huo Wagala waliwazidi nguvu, jambo ambalo lilisababisha Wambokomu kugawanyika katika makundi matano ambayo ni Wachonyi, Waribe, Waduruma na Wagiriama (waliyobaki Kenya) huku Wadigo wakisambaa na kufanya makazi kuanzia mto Garise inchini Kenya hadi Lungalunga na kisha wakaingia Tanganyika kuanzia Horohoro hadi Tanga.
Kama ilivyo kwa makabila mengine ya Kibatu, Wadigo wanajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara hususan mahindi, mpunga, muhogo, mboga na matunda. Wanalima korosho kama zao kuu la biashara pia minazi kwa ajili ya chakula na biashara. Wadigo pia ni wafugaji wa ng’ombe, mbuzi na kuku.
Wanawake wa Kidigo wana kipaji katika masuala ya sanaa za mikono na hutumia vipaji hivyo kusuka mikeka, majamvi na vikapu. Ili kuongeza kipato Wadigo hujihusisha pia na uvuvi, na biashara ndogo ndogo.Waliongozwa na mtawala aliyeitwa Bandilo.
 Mtawala huyo aliheshimiwa sana kwa kuwa alikuwa hodari katika matumizi ya mishale pia alikuwa na utaalamu wa dawa za asili na kutabiri matukio mbalimbali.
Kazi ya utabiri na utabibu ilisababisha mtawala huyo kuheshimiwa pia na watawala wa makabila mengine ambao walifika kwake kufanya utabiri na kutafuta suluhu za matatizo mbalimbali yanayohitaji maamuzi magumu.
Historia kwa njia ya simulizi inasema karne ya 20 Wadigo walikuwa na desturi za pekee tofauti na wakazi wengine wa pwani. Nyumba zao za asili zinaitwa Msonge.
Nyumba hizo zenye umbo la duara ni kubwa kwa wastani, hujegwa kwa miti na udongo na kuezekwa kwa nyasi. Nyumba hiyo huwa na vyumba viwili na sebule moja kwa ajili ya kulala wavulana.
Chumba cha wasichana hutumika pia kama jiko na kuwa katikati ya chumba cha wazazi na chumba cha wavulana ambacho pia hutumika kama sebule. Hata hivyo, Wadigo wamebadilisha mfumo wa maisha na hivi sasa wanajenga nyumba za kisasa zenye vyumba zaidi ya vitatu.
Walikuwa na miiko mbalimbali inayowatofautisha na makabila mengine. Kwa mfano, ikiwa kijana wa kiume amefanikiwa kujenga nyumba na kufariki kabla ya kuoa ni lazima kufanyike tambiko maalumu ili kuzuia balaa kwa vijana wengine.
Kabla ya kuzikwa anaingizwa kwenye nyumba yake mpya na kuombewa kisha kwenda kuzikwa. Ikiwa kijana huyo atafia mbali na kuzikwa mbali na nyumbani kwao basi nyumba yake itabomolewa na kujengwa upya. Nyumba mpya inapokamilika kundi la vijana ambao wameoa huhamia uko kwa pamoja na iliaminika kuwa wakihamia mmoja mmoja watapatwa na balaa.
Hata hivyo, imani hiyo imemalizwa na kuenea kwa dini ya Kiislamu na dini ya Kikristo miongoni mwa jamii ya Wadigo. Pia walikuwa na miiko kuhusiana na mapishi na chakula. Wakati wa kupika ilikuwa mwiko kwa mwanamume kuingia jikoni na wakati wa kula wanawake hawakuruhusiwa kujumuika na waume zao.
Wanawake walikula wakiwa jikoni pamoja na watoto wao wa kike na wanaume walikaa sebuleni pamoja na watoto wao wa kiume. Hata hivyo, mambo yamebadilika, siku hizi, baadhi ya wanaume huwasaidia wake zao kupika.Pia baadhi ya familia za Kidigo na watoto wao wa kike na wa kiume wanaweza kuchanganyika wakati wa kula.
Pia baba na mama wanaweza kukaa na kula pamoja na watoto wao. Kama ilivyo kwa makabila mengine ya Kiafrika, Wadigo walikuwa na imani ya kipekee kabla ya kuingia dini ya Kikristo na Kiislamu.
 Waliamini mizimu ya babu zao maarufu kwa jina la Madibwe au Adibwe. Waliamini kuwa mtu akifa hubadilika na kuwa na nguvu ya kipekee inayoweza kulinda au kusumbua binadamu. Ili kuimarisha amani katika jamii mtawala wao maarufu kama Bandiwe alitenga siku maalumu ya kufanya tambiko la kuomba amani na baraka.
Siku ya tambiko Bandiwe alivaa mavazi rasmi na kufanya sala ambayo huambatana na sherehe kubwa. Katika sherehe hiyo watu walikusanyika wakiwa wamebeba majembe na mikuki kisha kula, kunywa na kucheza ngoma.
Mwandishi Kayamba anasema ingawa hakuna mtu anayependa kufa inaelezwa kuwa Wadigo ni miongoni mwa makabila yanayoogopa sana kifo. Ingawa wanaamini kila anayezaliwa lazima ataonja mauti hupenda kutafuta sababu ya kifo jambo linalosababisha baadhi ya ndugu, jamaa na mafariki kufarakana kutokana na imani ya uchawi ambapo kila kundi hujaribu kutafuta sababu ya kifo cha mpendwa wao.
Wadigo walikuwa na desturi ya kugawana majukumu katika malezi ya vijana ambapo akinamama huwafundisha wasichana juu ya majukumu ya kutunza familia na wanaume waliwafundisha wavulana juu ya jukumu la kulinda na kuongoza familia. ningependa kusikia maoni yako asante sana kwa kufuata ukurasa huu kuhusiana na hii taarifa ya Historia Ya Wadigo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *