Afya

Maelezo kuhusu Chembe Cha Moyo na matibabu yake ( Angina pectoris)

MAELEZO KUHUSU CHEMBE YA MOYO NA MATIBABU YAKE (ANGINA PECTORIS)

Chembe ya moyo hujumuisha dalili mbali mbali ambazo huashiria kukosekana kwa hewa safi ya oxygen kwenye misuli ya moyo. Dalili kubwa zaidi ya chembe ya moyo ni maumivu ya kifua na kuwa na pumzi fupi.

Chembe ya moyo sio ugonjwa lakini ni moja ya dalili zinazoashiria uwepo wa magonjwa kwenye mishipa ya damu izungukayo moyo, ambapo kunakosekana usawa kati ya uhitaji na upatikanaji wa hewa safi kwenye moyo.

Dalili za chembe ya moyo hujumuisha maumivu ya kifua, pumzi fupi, kuhisi uwepo wa kitu kizito sehemu ya kifuani, kuhisi kuelemewa upande mmoja, kuhisi kuungua maeneo ya kifuani, maumivu ya meno, kuhisi kuvutwa na kamba kifuani, kuhisi uwepo wa kitu maeneo ya kooni n.k

Upungufu wa hewa safi ya oxygen hutokea mara baada ya kupungua kwa damu kuzunguka moyo.

Chembe ya moyo hutokea endapo mahitaji ya hewa safi yakiongezeka zaidi. Kuna sababu nyingi za kuongezeka kwa mahitaji haya ya hewa safi ya oxygen ambayo ni kuvunjika au kufungwa kwa mishipa izungukao moyo, kupungua kwa upana wa mishipa ya damu, kuganda kwa mafuta katika mishipa ya damu.

Kupungua kwa hewa safi ya oxygen kwa muda mrefu hupelekea chembe hai au seli za sehemu ya moyo kufa. Chembe ya moyo inaweza kuwa yenye hatari endapo kuna uwepo wa magonjwa mengine ambatanishi ambayo ni shinikizo la damu, upungufu wa damu.

AINA ZA CHEMBE YA MOYO

(1) Aina ya kwanza (stable angina): Aina hii ya chembe ya moyo ina tabia zifuatazo;

▪️Ni yenye kudumu kwa kipindi kirefu

▪️Yenye kujirudia mara kwa mara katikati ya mwezi au mwaka. Maumivu ya aina hii ya chembe ya moyo ni yenye uzito mkubwa lakini hayajii kwa haraka na mara nyingi hupelekea kuona kama kuna kitu kizito kwenye kifua ambacho huambatana na hisia za kuungua kifuani na pumzi kuwa fupi.

Aina hii ya chembe ya moyo hudumu kati ya dakika 0.5 hadi 3, ijapokuwa kutoweka kwa haraka zaidi endapo mgonjwa akitumia kidonge cha kuweka chini ya ulimi cha nitroglycerin.

Aina hii ya chembe ya moyo husababishwa na kufunga au kuvunjika kwa mishipa ya damu izungukao moyo. Hivyo kwa mishipa ambayo haijafunga au kuvunjika yenye damu safi ya oxygen hushindwa kusukuma damu yenye kukidhi mahitaji ya moyo hasa kwa nyakati za mazoezi, mawazo au habari mbaya, kuwepo katika mazingira ya baridi na mara baada ya kula chakula kingi.

Watu ambao wapo katika hatari ya kuwa na aina hii ya chembe ya moyo ni wenye shinikizo la damu, mwenye mafuta mengi mwilini, uvutaji wa sigara, wasiofanya mazoeI na wenyw uzito mkubwa.

(2)Aina ya pili (Unstable angina): Aina hii ya chembe ya moyo ina tabia zifuatazo:

Chembe ya moyo yenye maumivu makali yenye kuja haraka na yenye kujirudia rudia mara nyingi zaidi ikilinganishwa na aina ya kwanza, hutokea hata kama umetulia pasipo kujishughulisha

Aina hii ya chembe ya moyo hutokea mara baada ya kuundwa kwa kitu chenye mafuta katika mishipa ya damu izungukao moyo, na upana wa mishipa ya moyo kupungua ambayo hupelekea kufunga au kuvunjika kwa mishipa izungukao moyo hatimae hupelekea damu kutofika ya kutosha kuuzunguka moyo

Kupungua kwa hewa safi ya oxygen hupelekea chembe hai za misuli ya moyo kufa kwa asilimia (10%-20%). Lakini matibabu ya haraka husaidia zaidi kuepusha na uwezekano huu kwa 5% to 7%.

(3)Aina ya tatu (Prinzmetal’s): Ni mara chache sana kwa aina hii kutokea, ila hutokea mara baada ya mishipa izungukao moyo kupungua upana au kusinya hivyo huzuia mzunguko wa damu kuuzunguka moyo. Hali hii huwa yenye hatari zaidi endapo mishipa izungukao moyo ikifungwa au kuvunjika

Mgonjwa hulalamika kuwa na maumivu ya kifua hata akiwa amepumzika au akiwa anafanya kazi. Maumivu haya au ukosefu huu wa faraja hauwezi kutoweka licha ya kutumia dawa.

Chembe ya moyo ya aina hii endapo ikiendelea kutokea kwa kipindi kirefu hupelekea kutokea kwa mshituko wa moyo, hatimae kifo.

(4) Ukiachana na aina hizo tajwa juu, pia mgonjwa anaweza kukumbana na aina nyingine ya chembe ya moyo inayojulikana kama (nocturnal angina).

Aina hii ya chembe ya moyo hutokea zaidi nyakati za usiku, ambapo unaweza kumsaidia mgonjwa kwa kumlaza kitanda huku kichwa kikiwa kwenye mto au kitanda kuinuliwa sehemu ya kichwani.

Soma hii pia ( faida za majani ya mapera)

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *